Saturday, 29 February 2020

Wewe ni binadamu kweli?Uzembe na changamoto zako usizifichie kwenye neno MKOSI.......

Rafiki yangu na ndugu yangu pamoja na changamoto unazozipitia amini ipo sababu ya wewe kupitia hayo na tumia muda huu kuzifurahia na kushukuru kwani zinakufanya uwe imara kama utazitafutia ufumbuzi, lakini ukijaribu kuzikwepa zitakuja na nguvu ya ziada.....

Leo nataka tujadiliane swala ambalo naona watu wanajaribu kukimbia kivuri chao wenyewe kwa kuita wana mikosi, wamerogwa na maneno mengine mengi ya kuonyesha kwamba changamoto wanazozipitia hazisababishwi na wao.

Hebu chukulia mfano mtu amemaliza chuo kikuu na amesomea mambo yanayohusu kilimo au biashara lakini anaangaika Kila siku anatafuta kazi hapati?Mtu huyu Kila anavyojaribu kutuma maombi ya kazi akiulizwa swali linalohusiana na uzoefu anashangaa kwamba atapata wapi uzoefu wakati ndio ametoka chuoni? Ana "A" ya cheti na anafikiria ingefaa kumpa kazi, mtu huyu anatafuta Ajira lakini zipo nyingi lakini yeye husema ana mkosi.

Hebu fikiria mtu ameamka asubuhi na kuanza kuitembelea mitandao ya kijamii kisha baadaye anakuja kukumbuka alikuwa na kazi muhimu ya kufanya anaanza kukimbizana baadaye anapata ajari anaumia na kulazwa na kusema mkosi.

Fikiria mtu anapokea mshahara kidogo na anaona hauwezi kumfanya akatosheleza maisha yake, baadaye watu wa mikopo wanamwambia huwezi kuendelea bila mikopo lakini hawamwambii mikopo ipi itamfanya ajikwamuwe na maisha anaamuwa kuanza ujenzi au kutumia fedha ya mkopo kulipa ada ya shule ya Mtoto na baadaye maisha yanazidi kuwa magumu zaidi anasema ana mikosi.

Rafiki hiyo ni mifano michache sana ambayo inatuonyesha namna watu wanavyojificha kwenye majina ya kukimbia changamoto zao na pale wanapoacha kujionea huruma na kujifokea kwa uzembe wao ndipo maisha yao yanaanza kuonyesha matumaini, watakapoacha kuishi kwa viwango vya wengine ndipo mambo yataanza kuwa mazuri.

JE WEWE NI BINADAMU?
Rafiki yangu kuna maneno mengi tunayatumia Kila siku pasipo kufahamu yana maana gani,ulishawahi kusikia mtu anasema mtu fulani hana ubinadamu,hana utu na ni mnyama? Je nini tofauti ya mtu, binadamu na mnyama?

Rafiki mimi siyo mpenzi wa kuangalia Tv,lakini kutokana na kile ambacho nakitafuta na mke Wangu anakijuwa  nakitafuta amekuwa akiniambia pale kipindi kizuri kinapoendelea na kina mafunzo ya kujenga, basi siku moja aliniambia njoo umsikilize mwanasaikolojia, Teolojia na mwanafalsafa akitoa elimu inayohusu maneno matatu hapo juu nami nitakueleza maana zake kwa kifupi na wewe utajitambuwa upo upande gani.

"MNYAMA"
Mnyama ni kiumbe yeyote mwenye uwezo wa kufanya.Mfano ukimuelekeza kitu anatekeleza, ni Sawa na ng'ombe ukimuelekeza kulima analima, bosi wako akikupa maelekezo una uwezo wa kufanya, wanyama wa mwituni wana uwezo wa kujitafutia chakula, uwezo wa kufanya ni sifa ya mnyama, sasa mnyama binadamu anatofautina na mnyama mfugo kwasababu anaweza kutoa mapendekezo yake lakini hana uwezo wa kutoa maamuzi, angalia ni Mara ngapi umetoa mapendekezo ofisini, kwa serikali lakini hayajabadilisha kitu? Hali ya kukosa maamuzi ni tabia ambayo wanyama wanayo.

"UBINADAMU"
Hapa ndipo tunafikiri Kila mwanadamu ana ubinadamu kumbe binadamu ni jina tu lakini ili uitwe binadamu kwa sifa za binadamu ni lazima uwe mtu wa maamuzi, ukisema ndiyo inakuwa ndiyo kweli na ukisema hapana inakuwa hapana kweli, binadamu si mtu wa kupendekeza bila kuamuwa, yeye ni mtu wa kuamuwa nini afanye, binadamu hafanyi anafanikisha, chukulia mfano wa Fundi na Injinia, fundi anafanya lakini Injinia anafanikisha kwani yeye ndio unatoa maelekezo nini kifanyike.

"UTU"
Hapa rafiki ni hatua ya juu sana ya ukuu kwetu binadamu ambayo ukiifikia utafurahia maisha yako.Hapa unafikia kiwango ambacho husumbuliwi na mambo yaliyopita na huchanganywi na mambo yatarajiwayo, unafurahia wakati uliopo bila kuvurugwa na swala lolote, unapokea Kila kitu kama kilivyo, unashukuru kwa Kila kitu, unakuwa chanya kwa Kila kitu. Hapa tunatakiwa tufahamu kitu kimoja muhimu, kabla ya Adam na Eva kumuasi mungu tulikuwa na uzima wa milele lakini hatukupewa ujuzi, baada ya kumuasi mungu akatupa ujuzi na kutunyang'anya uzima hivyo utu ni kiwango kinachokalibina na uzima ndio maana watu wote ambao wanafikia kiwango cha utu majina yao hayafutiki hata baada ya kufa.

Bila shaka umejifunza rafiki yangu nenda kapigane na ubinadamu, pambana uwe na "Utu" na achana na hali za kuishi kama mnyama, usitumie tena neno mkosi kwani ni kichaka cha kufichia uzembe wako.

Endele kufungua kiungo cha;
https://Kinyagakelvin.blogspot.com kuna mengi utajifunza.

Ni Mimi Mwl.Kelvin Kinyaga
Kinyagakelvin162@gmail.com
0763766944.

Friday, 21 February 2020

Kafara haikwepeki kwenye mafanikio......

Rafiki yangu na mwanamafanikio hongera sana kwa kuchaguliwa kuiona siku hii nzuri ambayo kimazoea unaweza kuona ni kawaida ila ni bahati ya pekee sana tumeipata na tunapaswa kuitumia ipasavyo kwenye yale ya kusudi kwetu karibu tujifunze pamoja.

SHUHUDA
Rafiki Leo wakati nawasha simu yangu nimekuatana na ujumbe wa meseji unasomeka hivi.

"(666)Pole na matatizo tunakuona ujafanikiwa jiunge na mtandao mkubwa wa matajiri duniani (666)bila kutoa kafara piga 0757838723 kama unahitaji"

Rafiki unaweza kuona namna ujumbe huo unavyofahamu tabia za walio shindwa na wamebaki kutamani kufanikiwa bila ya kufahamu wafanye nini, wengi wanatamani mafanikio lakini hawako tayari kutoa kafara, sielewi neno kafara unalitafsiri vipi lakini tambuwa huwezi kufanikiwa bila ya kutoa kafara nitakueleza chini kwanini ni lazima utoe kafara. Lakini kabla hatujaona umuhimu wa kafara kwenye mafanikio tuone dhana ya kafara na maana yake.

Rafiki kabla sijafahamu kafara ni nini niliamini kafara ni kutoa ndugu na jamaa uwapendao kwa mizimu ili mizimu ikupatie utajiri na pengine aliyetuma ujumbe huo alikuwa anaamini unafahamu hivyo ndio maana akasema bila kutoa kafara je wewe unaamini nini? Je unaweza kwepa kafara na ukafanikiwa?

Kwangu neno KAFARA ninalitafsiri kama hali ya kuamua kuachana na mambo unayoyapenda na yasiyo na tija kwako na kuamua kufuata mambo usiyo yapenda na wakati mwingine yenye kuumiza ila yanakufanya uwe bora na ufanikiwe, Je kwa dhana hiyo utakuwa umeanza kunielewa nini nataka nikuambie.

Rafiki yangu ni vigumu sana kufikia mafanikio ya juu kwa kuendelea kufanya kawaida,kuchelewa kuamka kufuatilia mpira na ushabiki wa kisiasa, kuangalia TV muda mwingi, kwenda kwenye starehe muda wote, kupenda mapumziko kuliko kazi, kufanya matumizi kuzidi kipato na kukopa bila mipango na kutokuwa na tabia ya kujifunza na ukafanikiwa, rafiki kuachana na tabia hizo na zingine kama hizo unaweza kuona ni rahisi lakini sivyo kama udhaniavyo na hapa ndipo KAFARA inahitajika ndugu yangu lazima uwe tayari kuachana na vitu vingi unavyovipenda vosivyo na tija kwako nakufuata vitu vyenye tija hata kama huvipendi, toa kafara hiyo na mafanikio unayoyataka utayafikia kwa haraka.

Ni hayo rafiki yangu nenda katoe kafara Leo, futa yote yasiyo na tija kwako na weka yenye tija, kataa mapumziko yasiyo na maana kwako weka kazi na jitoe kweli kwa kile unachohitaji na wakati mwingine utadharauliwa na kupingwa lakini simama imara utafika na hiyo ndio kafara halisi na achana na zile kafara za kijinga ulizoaminishwa mwanzo.

Asante na karibu tena kwenye ukurasa huu.
Ni Mimi Mwl.Kelvin Kinyaga
Kinyagakelvin162@gmail.com
0763766944

Sunday, 16 February 2020

Baada ya kubadilisha umri unabadilisha nini?

Miaka 31 iliyopita tarehe na mwezi kama ya Leo alizaliwa Mtoto wa kiume wa mwisho kwa mama Ernester Mzena,Wazazi Wangu na Dada pamoja na kaka yangu ambaye alikuwa Mtoto pekee wa kiume kabla ya Mimi kuzaliwa na kufanya idadi ya watoto kuwa nane, yaani watoto sita wa kike na wawili wa kiume hakika ilikuwa siku ya furaha sana kwao, ninachotaka kuamini furaha waliyokuwa nayo Wazazi na ndugu zangu ni matumaini waliyokuwa nayo kwangu,wanaamini kuna nguvu kubwa ipo ndani mwangu Je Leo ndugu hawa wanaendelea kuweka matumaini hayo kwangu? Wanaamini kuwa Nina nguvu ya kubadilisha nini kutoka dhaifu kuwa imara? Au wamepoteza matumaini na hawaoni mchango wowote kwangu, nilipojaribu kupiga simu na kumuuliza mama yangu anaichukuliaje siku hii? Anasema anamshukuru mungu kwani safari ya malezi haikuwa rahisi, kupitia kuuguwa shida za Kila aina lakini Leo nimekuwa mkubwa anaona kama Zawadi, ikiwa haya yametoka kwa Mzazi Je Mimi najipa maoni gani? Mimi ni nani? Ni baba wa namna gani? Ni thamani gani natoa kwa wengine? Najiona wapi miaka mitano, kumi au zaidi? Je nimekata tamaa? Au bado ninaishi kusudi langu?

Kweli nimepokea pongezi kedekede za kubadilisha umri lakini swali ni Je badiliko la umri linaambatana na mabadiliko yapi?
Rafiki Nina majibu mengi kwa maswali haya lakini jibu moja ambalo Nina uhakika nalo ni kwamba sijakata tamaa pamoja na magumu ninayopitia, sijali maoni ya wengine kwangu ila Nina amini mimi ni mshindi, nakataa maisha ya mazoea na naongeza thamani zaidi kwa watu wanaonizunguka, nitasambaza upendo zaidi kwa wengine nikiamini upendo ndio dini ya kweli.

Rafiki haya ni yangu lakini usikubali kusherehekea badiliko la umri lisiloambatana na badiliko la thamani unayotoa kwa wengine.

Happy birthday Kelvin, mapambana yanaendelea mpaka kieleweke.

Usiache kutembelea page yangu ya USTAWI WA FIKRA na kujifunza mambo mazuri yatakayokuimarisha kifikra.

Ni mimi Mwl.Kelvin Kinyaga
Kinyagakelvin162@gmail.com
0763766944
Asante.

Saturday, 15 February 2020

Muda huu usigawe kwa wengine hata kama wanaununua kwa mabilion ya shilingi......

Rafiki hongera kwa kuendelea kuwa nami kupitia page yangu, bilashaka unaishi kusudi la maisha yako ndio maana huachi kujifunza, washindi wote wanafahamu siri ya ushindi ni kujifunza na kuweka kwenye matendo, karibu tuwe sote.......

Rafiki Kila mmoja wetu ni mshiriki wa kuuza au kununua kwa namna moja au nyingine na wote tunategemeana kwa namna moja au nyingine,wa kuuza anamtegemea wa kununua na wa kununua anamtegemea wa kuuza na hayo ndio yanaleta ladha ya maisha, pamoja na kutegemeana huku bado kuna upande una nufaika zaidi ya upande mwingine hasa kwenye kuuza au kununua muda.

Je wewe unauza au una nunua muda?
Pengine unaweza ukaanza kujiuliza ni duka gani linalouza muda? Na Je na nunua au nauzaje? Rafiki kwanza tukubaliane kwamba mungu ametugawia muda kwa usawa bila kumpunja yeyote, wote tuna masaa 24.Sasa swali unalotakiwa kujiuliza ni hayo masaa 24 unayatumia kwa ajiri yako au wengine? Kama ni kwa ajiri ya wengine ni masaa mangapi unatoa kwa ajiri ya wengine na mangapi unatoa kwa ajiri yako? kuuza Masaa yote kwa mtu ni tatizo na kutumia masaa yote kwa ajiri yako mwenyewe ni tatizo lazima ujifunze kuuza na kununua muda wako.Je ni wangapi wameuza muda wao kwa Bakresah,hivyo muda mwingi hufanya kazi na kutumia ujuzi wao kwa manufaa ya bakresah? Hili siyo ninalotaka kukuambia rafiki au nataka kukukataza usiuze muda wako, pengine umeuza kwa serikali endelea kuuza kwani mwanzo lazima uuze halafu baadaye utaanza kununua lakini yapo masaa ambayo hutakiwi kuuza Je unataka kuyafahamu masaa hayo? Na ni kwa namna gani yatakufikisha kilele? Karibu.....

Muda huu usiuze kwa yeyote.
Rafiki haijarishi unakouza muda wako unalipwa shilingi ngapi lakini bila kutumia muda kwa ajiri yako mwenyewe hutayafikia mafanikio ya juu. Muda huo ni saa moja mpaka mawili baada ya kuamka na saa moja mpaka mawili baada ya kutoka kwenye shughuli zako za kipato kikuu,masaa ya asubuhi yatumie kuipangilia siku yako na namna utaiendea siku hiyo na yapi utayafanya kwa viwango vya juu kwa utoafauti na ulivyofanya Jana,maana usitarajie kupata matokeo tofauti kwa kufanya kitu kilekile na kwa namna ile ile. Masaa mawili na zaidi yatumie kwa ajiri yako, kwanza tathimin siku yako uliyoimaliza imemalizikaje? Yapi umefanya sahihi na yapi umekosea? yapi umekamilisha na yapi hujakamilisha na jipe sababu sahihi za kutokamilisha, nasema sababu sahihi kwani nafahamu mwili utakavyokupa sababu za kizembe zitakazo kubakiza ulipo bila kupiga hatua yoyote na hapa mwanafalsafa EPICTETUS ana tuambia;

"Allow not sleep to close your are aried eyes, until you have reckoned up each day time deed:"where did I go wrong? What did I do?and what duty's left undone?From first to last review your acts and then reprove yourself for wretched (or cowardly) but rejoice in those done well" Discourses 3.10.2.2-3.

Hayo yote yanatupa umuhimu wa kutoimaliza siku yako bila kujifanyia tathimini mwenyewe, wengi uuza muda wao kwa masaa mengi kwa hela kidogo na masaa baada ya kuwafanyia kazi walio nunua muda hutumia masaa yaliyobaki kustarehe na pesa ambazo wakati mwingine siyo zao, wamekopa na kuendelea kuwa na mfumo huo siku zote, hivyo rafiki usikubali kuingia kwenye mtego, pangilia mchezo wako wa kuuza na kununua muda lakini tenga masaa kwa ajiri yako.

Asante sana rafiki na uwe na siku njema.
Ni Mimi Mwl.Kelvin Kinyaga
Kinyagakelvin162@gmail.com
0763766944.

Friday, 7 February 2020

Haya apa makosa kumi umekuwa unafanya na yamekuchelesha.



Rafiki yangu mshukuru mungu kwa kuweza kupata nafasi ya kusoma makala hii muhimu kwenye page hii ya USTAWI WA FIKRA itakayokwenda kubadilisha namna ya kufikiri kwako, Nina amini ukisoma na kufanyia kazi lazima maisha yako yabadilike na utapiga hatua za kukutoa hapo ulipo na kukufikisha hatua ya juu kimaendeleo,imani hii inatokana na ukweli kwamba hata Mimi yamenitoa sehemu moja kunipeleka sehemu nyingine bora zaidi.Karibu tuwe sote....

Rafiki kabla hatujakwenda kuangalia maeneo hayo kumi utakubaliana na Mimi kwamba namna ya kufikiri kwetu ndio kunaleta shida kwenye maisha yetu, hivyo kwa kujifunza na kubadilisha namna ya kufikiri na kuamini ndio kunaweza kutuimarisha kuwa bora zaidi, sasa karibu ujifunze makosa kumi ambayo umekuwa unafanya kwa kujuwa au kutofahamu na yamekuwa yakikuangusha sana.

1.Eneo la kwanza ni hufahamu kusudi la maisha yako.
Rafiki yangu safari yoyote inaanza kama anayesafiri anafahamu ni wapi anakoelekea. Sasa kama mtu hajuwi kusudi la maisha yake na kwamba nini anataka na nini hataki basi hawezi fika popote kwenye ulimwengu huu wenye Kila kitu, kama unataka kufanikiwa basi juwa nini kitafanya ufanikiwe na kifuate na siyo Kila siku unakimbizana na fursa, Leo umesikia ufugaji upo,kesho umesikia kilimo unaacha kufuga na kuanza kilimo, huko ni kutojuwa kusudi la maisha yako.

2.Eneo la pili ni kulalamikia wengine kuwa sababu ya kushindwa kwako.
Ni kawaida kabisa kumkuta mtu akisema ni kwasababu sikupelekwa shule nzuri na Wazazi ndio maana maisha yangu yamekuwa ya shida,sababu Mimi ni yatima,Kwasababu serikali imegoma kuongeza mshahara, kama unatabia ya kulalamikia wengine basi tambuwa hutokosa na ndio utazidi kutofanikiwa, werevu wote uanza kuona tatizo ni wao hivyo hurekebisha kasoro zao na kupiga hatua.

3.Kuamini kwamba huwezi kufanya biashara kwani huna mtaji na biashara ndogo hazitakufikisha popote hivyo siku zote una amini utaanza biashara kwa kukopa au kwakuwa na hela nyingi ni kujichelewesha na hata ukipata hizo fedha nyingi biashara itakushinda na utakata tamaa ya kufanya biashara, anza na kidogo kisha kikuze ni njia nzuri ya kujifunza.

4.Kosa la nne ni kuona fahari kuwasaidia ndugu zako kifedha badala ya kuwapa elimu ya namna ya kupata fedha na wakajitegemea,kuna wangapi walikuwa msaada kwa ndugu zao na walipoanguka ki uchumi na familia zao zikaanguka? Kama ni Wazazi kijijini wape miradi ya kuku wafuge kuliko kuruhusu wakutegemee Kila siku watakunyanyua pale utakapoanguka. Hawahitaji msaada wa fedha wanahitaji mawazo ya kuwafanya wapate fedha na wajitegemee.

5.Kosa la tano unalofanya ni kukosa elimu ya fedha.
Rafiki hata kama umesomea uchumi, umesoma sana nikuambia kitu kimoja bado huna muelewa mpana wa mambo ya fedha, eneo la uwekezaji,akiba, mikopo mizuri na mibaya na fursa unazoweza kuziona bado hujaambiwa kwa elimu ya darasani kama unahitaji vitabu vizuri vitakavyo kuelimisha namna ya kukua kifedha.

6.Kuishi maisha bila bajeti.
Eneo hili linawatesa wengi sana, watu wananunua vitu kwa tamaa, hawapangi bajeti, hivyo ujikuta Kila siku kwenye madeni kwasababu hununua vitu wasivyovihitaji kwa pesa ambazo hawana.

7.Eneo la saba ambalo linakurudisha nyuma ni kuishi kwa kujifananisha na wengine.
Hapa rafiki panawatesa wengi, watu wamekuwa hawajipi maisha ya furaha kwasababu wanaishi viwango visivyo vyao,jirani kapeleka Mtoto shule nzuri ya gharama na Mimi nitakopa mwanangu aende shule nzuri, hivyo hujikuta kwenye msongo wa mawazo bila sababu.

8.Eneo lingine ambalo wengi linatutesa ni kufanya maamuzi kwa hisia;
Sisi binadamu tunapaswa kufanya maamuzi kwa kufikiri na siyo kwa hisia lakini Mara nyingi tunazipa hisia nafasi ya kutuamulia na hivyo kujikuta tukijutia maamuzi yetu,watu wanafahamu vyakula vinavyowaletea matatizo ya afya lakini wanaendelea kula kwa mazoea.

9.Eneo lingine ambalo tunakosea ni kuruhusu watu wanaotuzunguka wawe washauri wetu.
Ni kawaida kwetu binadamubinadamu kuamini watu wa karibu kutushauri kwa mambo ambayo hawana uzoefu nayo, mambo ya fedha muone aliyefanikiwa kifedha atakushauri, mambo ya afya muone alibobea kwenye afya na siyo kupokea ushauri kwasababu ni ndugu au Wazazi.Kama unataka ushauri wowote nitakuunganisha na mtu sahihi karibu.

10.Kuamini kupata elimu ya darasi kutaamuwa hatma ya maisha yako.
Kizazi cha sasa kinawaza sana kwenye kuajiriwa kuliko kujiajiri, hivyo wasomi hukaa wakiamini na kusubiri ajira ambazo hazipo na kuweka maisha yasubiri wakati fursa zipo kibao Swala ni kuamka na kuzichangamkia.

Rafiki hayo ni maeneo kumi ambayo umekwenda nayo yamekuangusha,weka kazi na nidhamu binafsi na muda yafanyie kazi hayatakuacha hapo ulipo.

Makala hii imeandikwa na Mimi Mwl.Kelvin Kinyaga.
Nataka tufike wote juu usiache kufuatilia page hii Kila jumamosi. Asante sana.