Saturday, 29 February 2020

Wewe ni binadamu kweli?Uzembe na changamoto zako usizifichie kwenye neno MKOSI.......

Rafiki yangu na ndugu yangu pamoja na changamoto unazozipitia amini ipo sababu ya wewe kupitia hayo na tumia muda huu kuzifurahia na kushukuru kwani zinakufanya uwe imara kama utazitafutia ufumbuzi, lakini ukijaribu kuzikwepa zitakuja na nguvu ya ziada.....

Leo nataka tujadiliane swala ambalo naona watu wanajaribu kukimbia kivuri chao wenyewe kwa kuita wana mikosi, wamerogwa na maneno mengine mengi ya kuonyesha kwamba changamoto wanazozipitia hazisababishwi na wao.

Hebu chukulia mfano mtu amemaliza chuo kikuu na amesomea mambo yanayohusu kilimo au biashara lakini anaangaika Kila siku anatafuta kazi hapati?Mtu huyu Kila anavyojaribu kutuma maombi ya kazi akiulizwa swali linalohusiana na uzoefu anashangaa kwamba atapata wapi uzoefu wakati ndio ametoka chuoni? Ana "A" ya cheti na anafikiria ingefaa kumpa kazi, mtu huyu anatafuta Ajira lakini zipo nyingi lakini yeye husema ana mkosi.

Hebu fikiria mtu ameamka asubuhi na kuanza kuitembelea mitandao ya kijamii kisha baadaye anakuja kukumbuka alikuwa na kazi muhimu ya kufanya anaanza kukimbizana baadaye anapata ajari anaumia na kulazwa na kusema mkosi.

Fikiria mtu anapokea mshahara kidogo na anaona hauwezi kumfanya akatosheleza maisha yake, baadaye watu wa mikopo wanamwambia huwezi kuendelea bila mikopo lakini hawamwambii mikopo ipi itamfanya ajikwamuwe na maisha anaamuwa kuanza ujenzi au kutumia fedha ya mkopo kulipa ada ya shule ya Mtoto na baadaye maisha yanazidi kuwa magumu zaidi anasema ana mikosi.

Rafiki hiyo ni mifano michache sana ambayo inatuonyesha namna watu wanavyojificha kwenye majina ya kukimbia changamoto zao na pale wanapoacha kujionea huruma na kujifokea kwa uzembe wao ndipo maisha yao yanaanza kuonyesha matumaini, watakapoacha kuishi kwa viwango vya wengine ndipo mambo yataanza kuwa mazuri.

JE WEWE NI BINADAMU?
Rafiki yangu kuna maneno mengi tunayatumia Kila siku pasipo kufahamu yana maana gani,ulishawahi kusikia mtu anasema mtu fulani hana ubinadamu,hana utu na ni mnyama? Je nini tofauti ya mtu, binadamu na mnyama?

Rafiki mimi siyo mpenzi wa kuangalia Tv,lakini kutokana na kile ambacho nakitafuta na mke Wangu anakijuwa  nakitafuta amekuwa akiniambia pale kipindi kizuri kinapoendelea na kina mafunzo ya kujenga, basi siku moja aliniambia njoo umsikilize mwanasaikolojia, Teolojia na mwanafalsafa akitoa elimu inayohusu maneno matatu hapo juu nami nitakueleza maana zake kwa kifupi na wewe utajitambuwa upo upande gani.

"MNYAMA"
Mnyama ni kiumbe yeyote mwenye uwezo wa kufanya.Mfano ukimuelekeza kitu anatekeleza, ni Sawa na ng'ombe ukimuelekeza kulima analima, bosi wako akikupa maelekezo una uwezo wa kufanya, wanyama wa mwituni wana uwezo wa kujitafutia chakula, uwezo wa kufanya ni sifa ya mnyama, sasa mnyama binadamu anatofautina na mnyama mfugo kwasababu anaweza kutoa mapendekezo yake lakini hana uwezo wa kutoa maamuzi, angalia ni Mara ngapi umetoa mapendekezo ofisini, kwa serikali lakini hayajabadilisha kitu? Hali ya kukosa maamuzi ni tabia ambayo wanyama wanayo.

"UBINADAMU"
Hapa ndipo tunafikiri Kila mwanadamu ana ubinadamu kumbe binadamu ni jina tu lakini ili uitwe binadamu kwa sifa za binadamu ni lazima uwe mtu wa maamuzi, ukisema ndiyo inakuwa ndiyo kweli na ukisema hapana inakuwa hapana kweli, binadamu si mtu wa kupendekeza bila kuamuwa, yeye ni mtu wa kuamuwa nini afanye, binadamu hafanyi anafanikisha, chukulia mfano wa Fundi na Injinia, fundi anafanya lakini Injinia anafanikisha kwani yeye ndio unatoa maelekezo nini kifanyike.

"UTU"
Hapa rafiki ni hatua ya juu sana ya ukuu kwetu binadamu ambayo ukiifikia utafurahia maisha yako.Hapa unafikia kiwango ambacho husumbuliwi na mambo yaliyopita na huchanganywi na mambo yatarajiwayo, unafurahia wakati uliopo bila kuvurugwa na swala lolote, unapokea Kila kitu kama kilivyo, unashukuru kwa Kila kitu, unakuwa chanya kwa Kila kitu. Hapa tunatakiwa tufahamu kitu kimoja muhimu, kabla ya Adam na Eva kumuasi mungu tulikuwa na uzima wa milele lakini hatukupewa ujuzi, baada ya kumuasi mungu akatupa ujuzi na kutunyang'anya uzima hivyo utu ni kiwango kinachokalibina na uzima ndio maana watu wote ambao wanafikia kiwango cha utu majina yao hayafutiki hata baada ya kufa.

Bila shaka umejifunza rafiki yangu nenda kapigane na ubinadamu, pambana uwe na "Utu" na achana na hali za kuishi kama mnyama, usitumie tena neno mkosi kwani ni kichaka cha kufichia uzembe wako.

Endele kufungua kiungo cha;
https://Kinyagakelvin.blogspot.com kuna mengi utajifunza.

Ni Mimi Mwl.Kelvin Kinyaga
Kinyagakelvin162@gmail.com
0763766944.

No comments:

Post a Comment