Saturday, 9 May 2020
Njia unaifahamu lakini hauko tayari kwenda...........
Rafiki yangu hongera kwa siku nyingine, shukrani nyingi sana kwa mwenyezi mungu kuendelea kutupa sababu ya kuishi, bilashaka yapo tunayopaswa kukamilisha ndio maana tunaendelea kuwa hai,karibu rafiki tuweze kushirikishana machache ili tuweze kupunguzia mateso yaliyo msingi wa maisha yetu.
1.UBONGO
Rafiki yangu pengine ulishawahi kujiuliza au kutaka watu wote wafanye yaliyo sahihi pekee wasikosee kwa lolote,hata wewe ulishawahi kutamani usikosee kwa lolote, uachane na Tabia mbaya usiyoipenda kwako mwenyewe hasa linapokuja swala la fedha, pengine ni kukopa na madeni yamekuchosha lakini huwezi toka na kuachana na madeni na unaendelea kukopa pamoja na matatizo unayopitia, ulishajiuliza ni kwanini? Basi zipo sababu nyingi lakini hebu tuangalie sababu mbili zinazotutesa wengi.
A.Kwasababu hutaki kuonekana umeshindwa; hapa unaweza usinielewe ni kwa vipi? Mara nyingi tunapojaribu vitu vipya tunaanza na kushindwa, pengine unafahamu kabisa njia ya kuongeza kipato ni biashara lakini kwakuwa biashara siyo kitu rahisi hivyo kwa kuangalia wanaoshindwa na wewe hutaki kujaribu, pengine umekuwa una mazoea ya kukutana na rafiki zako Kila mwisho wa wiki kwa ajiri ya starehe na sasa unahitaji kuachana na mwenendo huo ili ufanikiwe unaona kwamba watu watakuona umeishiwa ndio maana upo tayari kuridhisha wengine ila si kwa manufaa yako, sisi binadamu ni wepesi kutengeneza tabia lakini wagumu kuzivunja hata kama zinatuumiza.
B.Sababu ya pili ni kukosa kusudi;neno hili kusudi siyo mara yako ya kwanza kulisikia lakini chochote ambacho ipo kusudi ya kufanya lazima utakifanya, hebu angalia ni wangapi wapo tayari kufa kwasababu ya njaa? Hivyo sababu lipo kusudi la kwamba wanataka kuishi lazima wajitoe kupata chakula. Kwenye kitabu cha MAN'S SERCH FOR MEANING cha Viktor Frankly anasema zipo hatua za kufuata ili kutengeneza kusudi,Lazima uwe tayari kufanya njia za kibunifu kwani unapotaka kufanya kitu lazima ufahamu kuna kupingwa,kukataliwa, kukosolewa na kukatishwa tamaa hivyo kama huna ubunifu huwezi kuendelea, Lazima kuwe na kitu unachokijali sana,pengine ni familia yako, la mwisho lazima ukubali kuteseka kwani mateso ndio msingi wa maisha ya kusudi, hivyo huwezi pata unachotaka kirahisi. Chukulia mfano wa mtu anayejifunza kuendesha baiskeri, Je anaweza chukuwa baisker kwa mara ya kwanza na kuendesha bila kupitia kikwazo chochote? haijarishi utafahamu njia zote za kuendesha baiskeri lazima utakapoanza kujifunza utajaribu na kushindwa na kuanguka, utachekwa lakini utapambana mpaka uweze hivyo usiogope kujaribu vitu vipya kwasababu ya kushindwa, kataa mazoea na usihofu unapojaribu na kushindwa, ng'ang'ana mpaka upate unachotaka.
2.VITABU VINNE
A.THINK AND GROW RICH-Kimeandikwa na Napoleon Hill mwaka 1935,mwandishi ametumia zaidi ya miaka 25 na kugundua kwamba mafanikio yoyote yanaanza na wazo, malengo ya kulitimiza wazo hilo,kisha uvumilivu na shauku vitafanya ufikie kile unachohitaji,mwandishi anamtumia mtu mmoja ambaye anaitwa Edwin, hakuwa na chochote ila alikuwa na shauku ya kufanya kazi na mtu maarufu (Thomas Edison)mtu aliyegundua taa za Umeme, pamoja na kuwa hakuwa na chochote lakini shauku yake ilipelekea kuajiriwa na Thomas na mwisho wa siku kufanya nae kazi, Je wewe unayo shauku ya kitu gani? Je shauku yako imeambatana na uvumilivu gani?usifute wazo lako Bali badili mbinu za kulifikia wazo lako, tutendelea kukichambuwa kitabu hiki na utajifunza mengi.
B.THE RICHEST MAN IN BABYLON;Kitabu kimeandikwa na George S Clason; kitabu kiliandikwa mwaka 1920,wote tunafahamu historia ya mji wa babeli, mwandishi anasema kanuni za fedha ziliazia babeli na Leo duniani kote tunazitumia, kitabu hiki kimesomwa na matajiri wengi duniani na kupitia kitabu hiki watu wameweza kufikia mafanikio ya juu sana,mwandishi anaanza kwa kusema maendeleo ya mtu mmoja mmoja ndio yanaleta maendeleo ya taifa zima, wengi tunaamini taifa ndio linaendelea kisha watu wake ndio wanaendelea lakini hili siyo kweli, hebu tujiulize kupitia matajiri unao wafahamu wewe ni Kodi kiasi gani serikali inakusanya? Na kulipa wafanyakazi wake serikalini? Je matajiri hawa wameajiri watu wangapi? Je Kila mtu angefahamu mbinu za kuupata utajiri na kuzifuata taifa letu lingekuwa wapi? Mwandishi anasema hivi,"OUR ACTS CAN BE NO WISER THAN OUR THOUGHTS.OUR THIKING CAN BE NO WISER THAN OUR UNDERSTANDING" akiwa na maana kwamba matendo yetu hayawezi kuwa mazuri zaidi ya mawazo yetu. Mawazo yetu hayawezi kuwa mazuri zaidi ya uelewa wetu. Hapa tunaweza kuona namna muunganiko wa mawazo, matendo na uelewa unavyohitajika ili tuweze kufikia ndoto zetu.
C.RICH DAD,POOR DAD;Kimeandikwa na Robert Kiyosaki, kitabu hiki kinatupa elimu namna maisha halisia yalivyotofauti na yale tunayojifunza shuleni, mwandishi anatupa ufafanuzi kupitia baba zake wawili, ambapo baba zake hao wote wawili wanampa funzo la maisha, baba zake hawa wawili walifanana kwenye Kila kitu isipokuwa upande wa fedha, baba tajiri ambaye alisoma na kuishia darasa la nane na baba masikini alisoma na kufika ngazi ya juu ya elimu yaani PHD au shahada ya uzamivu, baba huyu msomi ndio alikuwa baba yake Mzazi na baba wa rafiki yake aliyeishia darasa la nane alikuwa tajiri, baba msomi aliamini fedha ndio chanzo cha matatizo wakati baba tajiri aliamini kutokuwa na fedha ndio chanzo cha matatizo, mmoja aliamini ukienda shule unapata kazi nzuri na baba tajiri aliamini ukienda shule ili uje kumiliki kampuni yako, Mmoja anaamini kuwa na watoto ndio sababu ya kuwa tajiri,wakati mwingine aliamini kuwa na watoto ndio sababu ya kutokuwa na utajiri, hivyo pamoja na sababu hizi kuwa kwenye kitabu hiki lakini hizi ndizo sababu zilizopo mtaani kwetu, wangapi wanajilaumu kutofanikiwa kwasababu ya kuwasomesha watoto? Sehemu inayofuata tutajifunza masomo sita aliyojifunza Robert kutoka kwa baba Tajiri.
D.ELIMU YA MSINGI KUHUSU FEDHA;Kilichaondikwa na Dr.Amani Makirita, kitabu hiki kimeanza na kutoa maana ya fedha, wengi tunahangaika kupata fedha lakini hatufahamu maana yake, ni Sawa na kutafuta mtu usiyemfahamu, lakini Leo kupitia kitabu hiki mwandishi anataka kufahamu maana ya fedha, Fedha ni Njia ya Kubadilishana Thamani, hivyo fahamu kwamba unalipwa kulingana na thamani unayotoa, kama thamani yako ni 500 utalipwa 500,huwezi kupokea zaidi ya unachotoa.
Rafiki nitakwenda nikigusia maeneo baadhi ya vitabu hivi lakini ukitaka kupata kwa kina yaliyopo kwenye vitabu hivi nunua na uvisome mwenyewe.
3.KOCHA
Kutoka kwenye tafakari ambazo nazipata Kila siku kutoka kwa kocha ipo moja inasomeka hivi, Ukitaka kuwa juu ya wengine basi kuwa chini yao, kauli hii inatufundisha unyenyekevu, kama unataka kuwa na nguvu dhidi ya wengine basi jifunze kuwanyenyekea, na ili kufahamu hili namna linavyofanya kazi angalia Bahari inavyojinyenyekeza kwa mito, bahari ipo chini na mito ipo juu, lakini mito yote hupeleka Maji yake baharini na baadaye bahari inakuwa na nguvu kuliko mito, hivyo kama unataka chochote basi kuwa mnyenyekevu.
4.POROJO(Je hatua wanazozichukuwa serikali yetu ni sahihi dhidi ya gonjwa hili?)
Wiki hii nilipokea meseji kutoka kwa rafiki yangu akinitaka nieleze nimelichukuliaje swala la Corona na hatua Serikali yetu inazozichukuwa? Rafiki hizi ndizo porojo zinazoendelea mtaani kwa sasa, sikuwa na jibu zaidi ya hili,Serikali ipo sahihi au haipo sahihi hili si muhimu sana bali Mimi mwinyewe hatua ninazozichukuwa dhidi ya Corona ni sahihi au siyo sahihi?watu wengi tunafahamu kama maamuzi ya wengine ni sahihi au siyo sahihi ila hatufahamu maamuzi yetu kama ni sahihi au siyo sahihi, hivyo achana kubishana na wengine bishana na wewe mwenyewe.
Rafiki makala hii imeletwa kwako na Mwl Kelvin Kinyaga, funguwa kiungo hiki https://kinyagakelvin.blogspot.com na utapata makala nyingi za mafunzo, pia unaweza wasiliana nami kupitia;
Email yangu: Kinyagakelvin162@gmail.com au number za simu 0763766944
Kwa pamoja tutafika,Asante sana tutakutana wiki ijayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment