Wednesday, 22 July 2020
Gharama zilizojificha ambazo zinaongeza matumizi yako......
Hongera sana rafiki yangu kwa siku hii nyingine, Nina imani hujambo na waendelea na mipango yako mizuri ya Kila siku, endelea kuweka kazi kwani huyo ndio rafiki wa kweli na hawezi kukutupa.......
Leo tutaangalia sehemu ya matumizi ambayo wengi tunapoteza fedha zetu pasipokufahamu,au kuona ni kiasi kidogo lakini baada ya muda kupita tunakuwa tumepoteza kiasi kikubwa sana. Mwandishi anasema ni muhimu kufahamu kitu kinachochukuwa fedha kwenye mfuko wako kwani kadri matumizi yanavyoongezeka na kuwa makubwa ndivyo unavyojiweka mbali na utajiri. Na pale tutakapo dhibiti matumizi haya basi hata kiasi cha kujilipa kinaweza kuongezeka.
*Kundi la kwanza ni gharama za miamala ya kifedha*
Maisha yamekuwa rahisi sana,unaweza kukaa tu nyumbani kwako na kupata mahitaji yako yote muhimu ya kifedha. Urahisi huu umefanya tunapoteza fedha nyingi sana kwani huduma hizi nzuri zina gharama na kadri tunavyozitumia bila mipango ndivyo tunavyoingia gharama kubwa.
Hebu chukulia mfano mfanyakazi analipwa mshahara kupitia benki kisha akahamisha salio kwenye simu yake, akitaka kutoa itabidi aende kwa Wakala,hapo anakuwa amekatwa wakati anahamisha salio, kisha atakatwa kutoa fedha kwa Wakala na anapoteza takribani 10000 mpaka amepokea hela yake kama kiasi anachochukuwa ni laki moja kuendelea.Mwandishi anasema watu wengi hupenda kuacha fedha benki ili wasizitumie kirahisi lakini Kila wanapopata tatizo huenda Benki na kutoa salio na hapo kuongeza gharama, wengine huacha kwenye simu zao na kutoa kidogo kidogo na hapo pia gharama zinaongezeka. Kama una tabia za hivi nenda kachukuwe benki statement na utaona kiasi unachopoteza.
_Hatua za kuchukuwa_
A.Acha kufurahia huduma piga hesabu zako vizuri
B.Toa fedha zako kwa Mara moja na jijengee nidhamu ya kutorudi tena benki baada ya kutoa kiasi chote ulichopangia bajeti bila kurudirudi benki.
C.Kama uko mbali na benki na hivyo kuokoa gharama ya usafiri basi toa kiwango kikubwa kwa Mara moja kuliko kutoa Mara kwa Mara.
D.Kama unalipwa kwa njia ya simu kwa kazi unazofanya basi usitoe Kila unapolipwa bali subiria mpaka zimekuwa nyingi uzitoe kwa pamoja.
E.Kabla hujatumia huduma za ATM na simu kwenye miamala jiulize kama hakuna uwezekano wa kutumia njia nyingine ili kupunguza gharama.
*Kundi la pili;gharama za mawasiliano*
Kwa sasa mitandao ya simu wamekuwa wakitumia Kila ujanja ili kuchukuwa fedha zako zaidi, zamani ulikuwa ukijiunga unapata kifurushi chenye Kila kitu lakini sasa hivi wanataka ukijiunga mb,basi itakubidi ujiunge na dakika peke yake na meseji pia peke yake, hili limechangia gharama kuongezeka, mwandishi anasema usipokuwa makini kwa mwezi utatumia zaidi ya 30,000 kwa vorcher pekee, gharama hizo siyo kubwa kama na wewe una nufaika na mawasiliano lakini kama hulipwi kwa mawasiliano kiasi ni kikubwa sana.
_Kitu cha kufanya kuepukana na gharama hizi_
A.Chagua mtandao mmoja Mkuu utakao tumia na ukakupatia huduma na vifurushi unavyotaka kuliko kuwa na mitandao mingi inayokuongezea gharama.
B.Tenga muda maalumu wa kuwasiliana na watu muhimu wote kwa Mara moja, kuliko kufanya mawasiliano ya Kila siku na kuongeza gharama.
C.Unapotumia mitandao ya kijamii kabla ya kufunguwa picha au video unazotaka kuangalia, vipo vitu Vingi vinavyokula mb za kutosha na havina msingi wowote kwako.
D.Kabla hujafanya mawasiliano jiulize kuna fedha nitapata, Je nita imarisha mahusiano? Ninatengeneza mtandao mzuri? Nje na hapo achana na mawasiliano hayo.
*Kundi la tatu; gharama ndogo ndogo za nyumbani*
A.Vifurushi vya TV;kama unalipa zaidi ya 10000 kwa king'amuzi basi umeamua kupoteza fedha zako kwa vitu vingi visivyo na tija.
B.Fuatilia kwa umakini gharama za Umeme na Maji.
C.Vyakula vinavyoharibika na kutupwa ni sehemu inayochukuwa fedha zako nyingine.
Wengi wanapuuzia maeneo hayo lakini umasikini wao unatokana na kupuuza kwao kwani fedha nyingi hupotelea hapa.
*Kundi la nne; Gharama ndogo ndogo za maeneo ya kazi na biashara*
Kuwa makini na vyakula au Vinywaji unavyotumia kwa kununua kwenye maeneo ya kazi, maeneo hayo yamekuwa yanachukuwa fedha nyingi pasipo kufahamu, kitu muhimu ni Maji ya kunywa ambayo unaweza chemsha nyumbani na kubeba kwenda nayo kazini. Hata chakula unaweza beba kama eneo la kazi halina utaratibu mzuri wa chakula na hili litakupunzia gharama.
Rafiki ukikaa chini na kufanyia kazi maeneo hayo, tayari unakuwa na kiasi ambacho unaweza kuongezea kwenye mafungu yako ya ki uwekezaji na kupiga hatua zaidi za ki maendeleo.
Asante sana na uwe na siku njema, makala hii imeandikwa na Mimi rafiki na Mwl.Kelvin Kinyaga, mwanafunzi wa namna fedha itaweza kunifanyia kazi kupitia chuo cha Kisima cha maarifa.
Kinyagakelvin162@gmail.com
https://kinyagakelvin.blogspot.com
0763766944/0712161251
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment