Wednesday, 15 July 2020
Jinsi ya kudhibiti matumizi yako na bado ukawa na maisha bora......
Rafiki yangu habari za wakati huu?, hongera kwa Zawadi ya maisha na kuweza kuifikia siku hii nzuri kabisa, ninaposema siku nzuri sijakubaguwa wewe unayepitia changamoto kwani Nina amini kwamba hayo unayopitia ndio uzuri wenyewe, uimara wa Kingo ya mtu unapimwa wakati wa mafuriko, mti imara utauona wakati wa dhoruba, hivyo kupitia changamoto siyo laana bali ni kipimo cha uimara wako na hivyo endelea kufurahia kwa lolote lile unalolipitia.......
Leo kutoka kitabu cha ELIMU YA MSINGI KUHUSU FEDHA tutaangalia namna ya kudhibiti matumizi yako na bado ukawa na maisha bora.
SIRI YA UTAJIRI NI UBAHILI,mwandishi ameanza na kauli hii kwa kusema watu wengi hupenda kuitumia. Na kupitia kauli hii kumefanya zoezi la kutengeneza utajiri kupewa taswira hasi. Kwasababu ubahili ni kubana sana fedha na kujinyima,na wengi wanaona hayo siyo maisha ya kuishi. Kwamba ni kwanini ujitese kutengeneza utajiri wa baadaye badala ya kuitumia fedha hiyo sasa na ukawa na maisha bora? Mwandishi anasema hili ni swali ambalo wengi hujiuliza na lina mantiki kwani hupaswi kuteseka leo ili kesho uwe na maisha mazuri.
Mwandishi anasema pamoja na kwamba kujitesa leo ili uishi maisha mazuri kesho siyo maamuzi sahihi lakini bado ukweli ni ule ule, matumizi yanapaswa kuwa madogo kuliko mapato. Lakini unalifikiaje hili huku ukiwa na maisha bora kabisa kwako, yasiyo ya kujitesa?
Swali unalopaswa kujiuliza hapa ni hili,kwenye mchakato wa kupata fedha na kuzitumia ni kitu gani unakijali sana? Kitu gani kinakupatia furaha wewe? Kwa kulifahamu hilo utaweza kudhibiti matumizi yako na huku ukiwa na maisha bora. Mwandishi anaitumia kauli inayopendwa sana kutumiwa na watu kwamba fedha haiwezi kununua furaha, kauli hii inatokana na watu kuahirisha maisha, wakiamini siku wakishakuwa na fedha basi ndio watakuwa na furaha,kitu ambacho hakiwezi kutokea. Mwandishi anataka tufahamu kitu kimoja kwamba fedha na furaha ni maeneo mawili tofauti kwenye maisha na yanaweza yasiwe na uhusiano wa utegemezi. Kitu muhimu kufahamu ni wewe kuwa na furaha kabla hata ya kuwa na fedha.
Tatizo la wengi wetu hatujuwi tunataka nini na kipi tunajali zaidi, tumekuwa tunaishi kwa matamanio na kujilinganisha na wengine pasipo kufahamu ni kipi hasa unachojali?na hili limekuwa linafanya tuishi kwa kutamani Kila kitu kwasababu tumeona wengine wanavyo, hapa mwandishi anatutaka tujifamu na kujitambuwa ni kipi tunataka kwenye maisha yetu na kuhakikisha kwa namna yoyote tunakipata. Na yale yote yasiyo na maana kwako unaachana nayo na hapo utakuwa na maisha ya furaha. Wakati nasoma hapa nikakumbuka maisha ya mama Theresa kwake umaana ulikuwa kusaidia wengine na alipomsaidia mtu aliona amepata furaha kubwa sana, upande wa Donald Trump yeye kwake furaha ilitokana na kumiliki majengo makubwa na kuyaandika jina lake Donald Trump na furaha huzidi pale jengo hilo linapokuwa refu kuliko majengo yote, kupitia watu hawa wawili tunajifunza kwamba pale unapofahamu nini hasa hitaji lako basi hakikisha unalipata, lakini hili halina maana kuweka hitaji lako kwa kile kilicho nje ya uwezo wako, huwezi kuwa huna mkono halafu ukataka muujiza utokee upate mkono ndio ufurahie, hivyo jiulize sasa hitaji lako ni nini? Mimi ninajisikia furaha kuzungukwa na watu wenye furaha na ndio maana Kila siku najitahidi wewe mtu wangu upate mafunzo yaliyo sahihi Je wewe ni kipi chenye maana na kukijali zaidi kwako?
Moja ya matajiri sana ambao wanasemekana ni bahili ni Bilionea Warren Buffet,ambaye wakati kitabu hiki kinaandikwa alikuwa tajiri namba mbili duniani na sasa ni namba tatu kama sijakosea, wakati kitabu hiki kinatolewa Julai 2019 tajiri huyu alikuwa na utajiri wa dola za kimarekani 77(kwa report za mwaka 2017) Sawa na zaidi ya Tsh trilioni zaidi ya 150,karibu Mara kumi ya bajeti ya nchi yetu ya Tanzania. Pamoja na utajiri wake huo bado anaishi kwenye nyumba yake aliyonunua mwaka 1958 huko Omaha, Nebraska nchini Marekani. Amekaa kwenye nyumba moja kwa zaidi ya miaka 62 sasa.Alipoulizwa kwanini pamoja na utajiri wake bado anaishi maisha ya kawaida? Akajibu mafanikio kwake ni kufanya kile kitu anachopenda na kwake ni kuwekeza.Hivyo hicho ndio kitu anafanya na vingine vyote havina nafasi, ingekuwa huku kwetu wangesema ni masharti ya mganga na Kila maneno.
Rafiki bilashaka unahitaji maisha yenye furaha, anza sasa kufahamu hitaji lako na pambana mpaka uweze kulipata na acha kukimbizana na Kila kitu.
Nikutakie siku njema, makala hii imeandikwa na Mimi rafiki yako Mwl.Kelvin Kinyaga; ninayo kushirikisha ni baadhi tu, mengi mazuri zaidi yapo kwenye kitabu hiki, tuwasiliane upate nakala yako.
Kinyagakelvin162@gmail.com
https://kinyagakelvin.blogspot.com
0763766944/0712161251
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment