Wednesday, 8 July 2020
Na hivi ndivyo unavyoweza kuyatumia mawazo yako mazuri uliyonayo kabla hujapata pesa........
Pale tunapogundua hakuna hongo wala sababu yoyote inayotufanya tuamke leo salama,haijalishi maumivu madogo madogo tuliyo nayo kutokana na mambo mbalimbalia ya nje lakini kitendo cha kutoa pumzi na kurudisha ndani ni kitendo cha kuanza siku hii kwa kumtukuza mungu wetu......
Karibu tena rafiki na ndugu yangu kwenye ukurasa huu ustawishe fikra zako, maana unahitaji ustawi wa fikra, ustawi wa kiroho pamoja na ustawi wa mwili ambao ndio hekalu linalobeba akili na roho zetu, ikiwa hata mwenyezi mungu mwenyewe alifahamu sisi watoto wake tunahangamia kwa kukosa maarifa je Mimi na wewe ni nani mpaka tuyapuuze?ili mwili na roho viwe salama vinahitaji akili timamu ambayo tunaipata kupitia maarifa.
Wiki iliyopita tuliangalia namna ya kugawa fedha zako kwenye mafungu yako na muhimu nikukumbushe tena, kama unahitaji kweli kufanikiwa basi lile fungu la tano ambalo ni matumizi yako,hakikisha haizidi asilimia sitini ya kipato chako. Leo tutajifunza namna ya kukaa na fedha zako hata pale unapozipokea kwa mkupuo tofauti na kiwango chako cha kimazoea unachokipokea siku zote.
Ni kawaida kwetu sisi binadamu kuwa na mipango mizuri kabla hatujapokea fedha, tukishapokea fedha mipango yote mizuri inapotea na kujikuta tukitumia fedha hizo kwa mambo mengine tofauti na mipango ya awali, hali hii imekuwa ikitesa watu wengi sana bila kufahamu sababu ni nini, kabla hatujaendelea na uchambuzi wa kitabu cha ELIMU YA MSINGI KUHUSU FEDHA nikuambie vitu vitatu ambavyo vimenisaidia sana kwenye fedha,vitu hivi nilijifunza mwaka 2018 kwenye semina ya kisima cha maarifa ya kufungua mwaka huu, nimekuwa navisema na nitaendelea kuvisema.
Moja;Kujenga misingi ya kutokopa, mipango yako ya kifedha imekuwa inavurugika sana kwasababu umekuwa mwepesi kukopa, akili ya binadamu inatabia ya kutafuta urahisi na kutoroka ugumu hivyo kama kuna namna ya kupatikana urahisi basi ukipata tatizo kidogo unakimbilia kutafuta njia ya mkato kwa kukopa, mkopo maana yake natumia fedha zangu kabla sijazipokea na nikizipokea narudisha kwa mwenye nazo, kabla hujakopa jiulize nani utalipa? Na atalipa kutoka wapi? Ni kweli wapo wengi sana wanaofanikiwa kwa kukopa lakini hawalipi kwa fedha zao huko mbele tukifika kwenye mikopo mizuri na mikopo mibaya tutayaangalia kwa kina.
Mbili;Jijengee msingi wa kutokopesha;watu wengi sana wameingia kwenye matatizo na watu hasa wanao wapenda kwa kudhani kwamba wakiwakopesha basi mahusiano yao yataimalika lakini baada ya watu hao kutowalipa ndipo mahusiano hayo yanakuwa mabaya zaidi, hivyo kama unataka kumkopesha mtu ambaye ni ndugu au rafiki wa karibu jiambie kiasi ninachompa hakiwezi kuharibu undugu wetu na urafiki hata asiporudisha fedha hii, hivyo mpatie huku ukijiambia hata kisipo rudi sitoathirika wala urafiki wetu na undugu hautavunjika, Mara nyingi tunao wakopesha tunawaongezea matatizo kuliko kuwasaidia kwani Leo akikopa kwako siyo kwamba matatizo yake ya kifedha ndio yatakwisha bali atakopa na kwa mwingine na mwingine na mwisho wa siku anasema ana pepo la madeni, kumbe tatizo ni nyie rafiki zake.Sijasema usisaidie ndugu au rafiki bali toa msaada usio athiri uhusiano wenu mambo yakienda kinyume.
Tatu;Tengeneza bajeti yako kabla hujapokea kipato chako na ukikipokea usitumie nje ya bajeti hiyo hata kingetokea nini, kama kitu ni muhimu kipangie bajeti kwenye kipato kinachofuata.
Kama utayaishi mambo haya matatu nina uhakika kabisa changamoto za kifedha utaondokana nazo Mara moja, ni sehemu niliyoifanyia kazi kwa haraka sana na siku zote nitaendelea kuamini safari yangu ya mafanikio nguzo zake kuu ni hizo tatu na nimeanza na eneo hilo kwani linahusiana na somo letu la Leo.
Ninawezaje kudhibiti kipato kikubwa kinachoingia kwa Mara moja?
Mwandishi anasema wapo watu wengi kulingana na kazi zao au hali fulani wanayofikia hujikuta wakipokea hela nyingi kwa mkupuo, pensheni kwa wastafu, wachimba madini, biashara ya udalali, kupokea urithi, lakini wakati mwingine hata Mimi na wewe tunapata pesa nyingi tofauti na kawaida na zinakwisha bila kufahamu zimeishaje Je tatizo ni nini hapo? Watu wamekuwa na mawazo mazuri kifedha wakiwa hawana fedha na wakizipata mawazo hayo upotea mpaka watumie ziishe ndio mawazo mazuri hurudi tena.
Mwandishi anasema watu wakiwa na fedha nyingi hupenda kupokea ushauri kwa Kila mtu bila ya kuchunguza ushauri huo anaopewa, na kwa wastafu hali hii upelekea hadi kifo cha mapema pale anapokuja kustuka fedha hizo zimetumika na kwisha bila kufahamu amefanyia nini. Yafuatayo ni mambo muhimu kufanya pale unapopata fedha nyingi kwa mkupuo.
1.Usijioneshe kwa wengine kwamba una kipato kikubwa.
Hapa mwandishi anasema binadamu hatuna siri ,maisha yetu yapo wazi sana. Ukifunga mdomo wako usiseme, matendo yako yanakuwa yanaongea waziwazi. Hili limekuwa linawagharimu watu wengi sana kwenye fedha. Kama watu wanaweza kufahamu kwamba sasa hivi unayo fedha na sasa hivi huna fedha basi wewe ni muhanga na somo hili linakuhusu. Rafiki watu wengi sana hawapendi kutafuta fedha kwa njia ngumu bali njia za mkato mkato hivyo wakishafahamu unayofedha watatumia Kila mbinu kujifanya wakikushauri kumbe hukuchukulia fedha zako, hivyo hakikisha ukiwa na fedha au ukiwa huna usomeki na unaonekana kawaida.
2.Hatua ya pili ni kugawa mafungu ya kipato hicho.
Kosa kubwa ambalo wengi wanafanya ni kutogawa fedha hizo kwenye mafungu ya matumizi na uwekezaji na hapo mwandishi anasema mipango inakuja kukumbukwa fedha zinapobaki kidogo. Anasema wengi wamekuwa wanafanya maamuzi mabaya ya uwekezaji kwa kutolea mfano wa mstaafu kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha kama sehemu ya kutengeneza kipato. Anasema huo ni uwekezaji mbovu kwasababu nyumba ambayo itahitaji mtu kuweka mpaka milioni 50 mpaka ikamilike unakuta kwa mwaka haiwezi kukupa zaidi ya milioni mbili na hapo hujaweka gharama ya kuifanyia marekebisho, huu ni uwekezaji unaolipa kidogo kidogo,kitu ambacho siyo rafiki pale mtu anapokuwa amestafu ndio atumie kama njia kuu ya kumuingizia kipato.
3.Wekeza kwenye mambo unayoyajua kwa kina na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wenye uzoefu.
Mwandishi anasema watu wengi wakiwa na fedha nyingi wanaweza kuwekeza kwa ushauri ambao unatoka kwa Mtoto wa darasa la saba. Mara nunua Bajaji zitakulipa au Lima nyanya zitakutoa, anasema watu wengi wanaweka mtaji wao mkubwa kwa ushauri wa namna hiyo.
Mwandishi anamalizia sehemu hii kwa kusema unapopata kiasi kikubwa kwa mkupuo basi tulia kwanza mpaka mihemko itulie na upate ushauri wa kitaalamu ndipo uwekeze fedha zako.
Na Mimi nasema kwanini usubiri yote hayo? Anza kuwekeza sehemu unayotaka kabla hata hujapokea penshen yako au kupokea fedha nyingi ili ukizipata ziingie kwenye kitu unachokifahamu, kama kuna biashara unapanga kuifanya kwa fedha za kustafia basi ianze sasa baada ya kupokea ushauri wa kitaalamu na siyo usubirie mpaka ulipwe kiinua mgongo utakuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza.
Nenda kayaweke kwenye vitendo rafiki yangu na nikuatakie siku njema. Asante nitaendelea kusamabaza upendo Wangu kwa kukupatia maarifa Kila siku.
kinyagakelvin162@gmail.com
https://kinyagakelvin.blogsport.com
Bonyeza maandishi haya kupata makala zote zilizopo kwenye ustawi wa fikra.
0763766944/0712161251
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment