Tuesday, 16 June 2020
Akili ya ndani katika safari ya mafanikio.......
Leo kabla sijakuambia nilichokuandalia naomba nikukumbushe kwamba hakuna chochote unachomiliki kwenye ulimwengu huu, vyote ulivyonavyo umeazimwa kwa muda na kuna siku mwenye navyo anaweza kuvichukua.Afya,Mali na utajiri, watu unao wapenda sana na chochote kile ulichonacho hata uhai wako umepewa kwa muda hivyo vipe thamani sasa ili vinapochukuliwa na aliyekupa usijutie na uwe imara kupokea matokeo.........
Rafiki yangu siku ya jumatano ni siku ambayo nakuchambulia kitabu cha THINK AND GROW RICH na hapa tunaangalia namna kufikiri kwetu kunavyosababisha ama tufanikiwe au kuendelea kuwa na maisha ya ufukara. Wiki iliyopita tuliona hatua tano za kufuata ili kujijengea uwezo wa kujiamini, nina imani ulizisoma na sasa hali ya kujiamini imeanza kujengeka, Leo tutaangalia aina za akili tulizonazo na namna zinavyofanya kazi.
Akili ya mwanadamu imegawanyika katika sehemu kuu tatu, yaani AKILI INAYOFIKIRI NA KUFANYA MAAMUZI(CONSCIOUS MIND),lakini pia ipo AKILI ISIYOFIKIRI WALA KUFANYA MAAMUZI ILA HUPOKEA TAARIFA INAYOINGIZWA (SUBCONSCIOUS MIND) na mwisho ni AKILI YA JUU KABISA INAYOTAWALA AKILI HIZI (SUPERCONSCIOUS MIND), hizi ndizo aina tatu za akili ambazo Kila binadamu anazo lakini namna tunavyoweza kuzitumia ndio kunatuletea utofauti.
Katika aina hizi tatu,akili ya ndani ambayo haifanyi maamuzi ina nguvu kubwa sana ya kuweza kupokea taarifa inayoingia kwenye akili yako.Pale taarifa hizo zinapofanywa kwa kujirudia rudia inatengeneza mambo hayo kuwa kweli. Hii ndio maana pale unapopokea sana taarifa zinazokujengea hofu ya kushindwa basi hali hiyo ya kushindwa itakuwa ikiendelea kwako na kama utajijengea mazingira ya kushinda basi hali hizo za kushinda zitaendelea.
Wakati nasoma eneo hili nilipata picha kubwa sana, Mimi kama mwalimu sitakiwi kumjengea mwanafunzi hali yoyote ya kumuonyesha yeye ni wa kushindwa hata kama anafanya vibaya kwenye mitiani yake, kwani hali hiyo ikijengeka kwenye akili yake anajiona ni wa kushindwa kwenye Kila kitu, vipi watoto zako hapo nyumbani? Nadhani sasa umeanza kuelewa kwani kama mwalimu wa DIAMOND alimwonyesha kwamba yeye ni wa kushindwa kwa kigezo cha mtihani sijuwi leo akikutana naye wanaongea nini?
Hivyo rafiki ipo njia ya kuitumia akili hii ya ndani na ikakufanyia kitu unachotaka, ipe amri akili yako ya ndani ili kutengeneza mazingira yatakayowezesha kufikia utajiri.Mwandishi anaita njia hii AUTO-SUGGESTION au SELF SUGGESTION hapa unaweza kuandika kwenye karatasi hitaji lako kubwa kwenye maisha yako na kulisoma Kila siku na kama utafanya hivyo huku ukiweka kazi na juhudi ya kupata kile unachotaka basi hakuna kitakachoshindikana,nimalizie kwa kumnukuu mwandishi hapa chini.
"Recall what has been said about the subconscious mind resembling a fertile garden spot,in which weeds will grow in abundance, if the seeds of more desirable crops are not sown there in"
Hivyo akili zetu za ndani ni mfano wa Shamba, kama utaliacha liwe na magugu hakuna mbegu itakayozaa ila ukilifanyia palizi na kuliwekea mbolea lazima litazaa na kustawi vizuri, hivyo kataa kabisa kauli hasi, hata kama wote watakuambia utashindwa wewe mwambie akili yako ya ndani hakuna kushindwa utanipa ninachotaka.
Asante sana rafiki na uwe na siku njema.
Kinyagakelvin162@gmail.com
https://kinyagakelvin.blogspot.com
0763766944/0712161251
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment