Sunday, 28 June 2020
Mambo matatu yatakayofanya msaidizi wako kwenye kazi ajitume.......
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri, siku ambayo tunamaliza wiki na kujiandaa kuanza lingine, kama ilivyokawaida yangu na nimekuwa naitumia kukushirikisha kwamba itumie siku hii kujifanyia tathimini ya kipi umefanya wiki hii kuiendea ndoto yako? Na kipi unapanga kukamilisha kwenye wiki unaloliendea? Yapi umefanya sahihi, yapi ulikosea na nimejifunza kupitia makosa hayo? Kwa kufanya hivyo kunakufanya uweze kujifunza na kutorudia makosa, lakini pia kunakufanya uongeze bidii kwenye kusudi lako unalofanyia kazi, karibu tuwe sote.....
Rafiki leo twende tukaangalie changamoto za wasaidizi wetu wa kazi kwenye shughuli zetu, lakini pamoja na majumbani.Kabla hatujaenda kuangalia ni vitu gani unapaswa kufanya ili waweze kujituma zaidi kwenye kazi zao hebu tuangalie ni kwanini nimesukumwa kuandaa somo hili.
Wakati naangalia changamoto kubwa ambazo nimezipitia wiki hii inayoisha ndipo nikagundua kama familia tuna angaika kupata mtu atakayeweza kukaa na wazazi wetu ambao ni wazee na wako kijijini, kwani wengi wamekuwa wanakaa kidogo na kuondoka lakini pamoja na kigezo na hitaji la wasaidizi hawa kutaka ongezeko la mshahara bado ufanisi wa kazi huwa ni mdogo na usioridhisha, wakati familia tunapitia kwenye changamoto hii lakini wiki hii pia tuliweza kukaa na wana partnership wa biashara tuliona changamoto ya Dada anayetusaidia kazi eneo la biashara kuwa na matatizo mengi yanayopunguza na kuathiri biashara yetu, uchelewaji, kiburi na kuleta mazoea kazini.
Baada ya kuona kwenye familia na kwenye biashara yetu tunapitia changamoto ya aina moja ndipo nikajitafakari kwa kina ni wapi tunaweza kuwa tunakosea, maana kuishia kulalamikia wasaidizi wetu bila ya kuangalia upande wetu ni kazi bure, baada ya kutafakari kwa kina nikakumbuka mwaka jana tulipata semina bora sana kwenye kisima cha maarifa kuhusu namna ya kukuza biashara zetu, hapo tulipata masomo kumi yenye Kila mafunzo kwenye biashara,baada ya kuanza kupitia ndipo niligundua kuna makosa mengi sana bado tunayafanya kwenye biashara na hata kwenye maeneo mengine yanayohusisha wasaidizi wa majukumu yetu, Kwenye semina ile somo la saba kati ya kumi lilisomeka hivi JINSI YA KUAJIRI WAFANYAKAZI WATAKAO WEZESHA BIASHARA YAKO KUKUA.
Wakati napitia somo hili niligundua makosa mengi tunayafanya wenyewe, tunapokuwa na uhitaji wa wasaidizi hakuna vigezo tunavyotumia kupima namna ya kuwapata bali tunaangalia tu kwamba tunahitaji mtu wa kutusaidia, lakini hata mtu huyo akipatikana tunaongea naye bila kuweka utaratibu wa ki maandishi wa orodha ya majukumu yake na namna gani utapima ufanisi wake, lakini pamoja na makosa hayo bado tukiona ameshindwa kutekeleza majukumu yake tunakimbilia kuwaondoa pasipo kuzungumza nao na kuwaambia ni nini tulitarajia kupata kutoka kwao na wapi wanakosea na kisha kuwapima tena kwa kuwashirikisha makosa wanayofanya na hili kupelekea Kila siku kuendelea kubaki kwenye changamoto hii kwa kufanya kwa namna tuliyozoea kufanya. Yako mengi sana nimejifunza hapa lakini twende tuone vitu vitatu vinavyofanya mfanyakazi ajitume zaidi kwenye majukumu uliyompangia.
1.Maamuzi(Autonomy)
Kufanya maamuzi ni kitu ambacho siyo rahisi sana kufanya kwa tulio wengi, watu hawa tunaofanya nao kazi wakigundua wewe msimamizi wao siyo mtu wa kufanya maamuzi bali ni mtu wa kuongea tu na huchukuwi hatua basi analeta mazoea ambayo yanakwenda ku athiri kazi au biashara yako, lakini ukiwa ni mtu mwenye msimamo na maamuzi lazima awe makini na kuweka kazi kwani anafahamu utamchukulia hatua Mara moja, hili linaanzia na namna yeye alivyopata nafasi hiyo.
2.Chenye maana kwake(Meaning)
Kama uliyemwajiri hakithamini kile anachopata kwenye kazi anayofanya iwe ni kwa kujifunza au kumsaidia kwenye maisha yake basi atakipuuza na kufanya kwa mazoea, lakini kama ataona kina maana kwake basi lazima aweke bidii, ipo njia ambayo itakusaidia kumfanya aone thamani na maana ya kile anachofanya ni kwa kumuonyesha manufaa atakayopata kama atajituma kwenye kazi na ukiona hilo anza kumpatia kitu cha ziada na kuonyesha unafurahishwa na jitiada zake.
3.Ukuaji(Growth)
Kama kile anachofanya msaidizi wako hakikui basi anachoka na kutoona kina umuhimu kwake, lakini akiona kinaelekea kukua na kuwa kitu kikubwa anaanza kuona atanufaika na ukuaji huo, hata ungekuwa wewe msomaji sehemu ambayo Kila siku iko vile vile haiongezeki na unapokea kiasi kidogo je utakaa?kaa naye na mshirikishe mwakani biashara itakuwa imefika wapi na je unataka miaka mitano ijayo biashara yako iwe imefika wapi na yeye atanufaikaje na mafanikio hayo, na Kila biashara inapokua na kukua basi iwe na muunganiko wa moja kwa moja na yeye.
Hayo ni machache kati ya vitu vingi ambavyo tumekuwa hatuviangalii kwa watu tunao waajiri na tumekuwa tukibaki kulalamika bila kuangalia upande wetu ni yapi tunayakosea, asante rafiki na uwe na siku njema.
Kinyagakelvin162@gmail.com
https://kinyagakelvin.blogspot.com
0763766944/0712161251
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment