Wednesday, 3 June 2020

Kila unachopitia ni wewe ndio umekivuta........



Rafiki yangu acha kuwaza matatizo yako muda wote, kwani kwa kufanya hivyo unaendelea kuyavuta matatizo kwako, jukumu lako ni kuwaza namna sahihi ya kuondokana na matatizo hayo kwa mtazamo chanya......

Rafiki yangu matokeo uliyonayo sasa husababishwa na namna unavyofikiri, ipo nguvu kubwa inayoendesha maisha yetu, dhana hii inaitwa nguvu ya mvutano (LAW OF ATTRACTION) Sheria hii inasema kwamba Kila kitu ambacho tunacho kwenye maisha yetu,tumekivuta sisi wenyewe. Kuanzia kwenye fedha, mke uliyenaye au mume,huzuni au furaha, utajiri au umasikini,na mambo mengine mengi, mfano marafiki ulio nao ni Tabia zako na namna unavyofikiri ndio kumewavuta kwako.

Rafiki yangu nguvu hii inakufanyia maamuzi mengi sana, kama unafikiria fedha ni nzuri basi unaivutia kwako lakini kama unafikiria fedha ni mbaya na ni chanzo cha uovu basi fedha inakaa mbali na wewe, Jana tuliona nguvu ya Imani, hivyo anza kuona uzuri uliopo kwenye fedha huku ukiweka bidii hilo litakufanya uivutie pesa na ona changamoto kama fursa na siyo matatizo. Jiulize NAWEZAJE KUPATA FEDHA na siyo SIWEZI KUPATA FEDHA HIZO kama kitu ni muhimu jiambie unawezaje kukipata.

Rafiki kwa kuwa na mtazamo sahihi kwenye fedha kunakufanya uzivutie fedha zaidi, hebu tuangalie sheria tano za fedha unazopaswa kuzifahamu. Kutoka kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI KUHUSU FEDHA mwandishi amezifafanua vizuri sana.Sheria hizi amezisoma kwenye kitabu cha The richest man in the Babylon ambacho nacho tunaendelea na uchambuzi wake.

1.Sheria ya kwanza ni KUJILIPA MWENYEWE;
Kanuni hii inasema kwamba fedha huenda kwa mtu ambaye anatenga siyo chini ya sehemu ya kumi ya kipato chake. Hii ni kwa ajili ya maisha ya baadaye, hapa ndipo ilipo dhana ya kujilipa wewe kwanza, unamlipa Kila mtu nqa kujisahau wewe mwenyewe, unamlipa muuza nguo, unamlipa fundi nyumba, unalipia Kila kitu na kujisahau wewe. Hivyo anza kutenga sehemu ya kumi ya kipato chako.

2.Sheria ya pili ni FEDHA KUKUFANYIA KAZI
Fedha hufanya kazi kwa juhudi kwa yule mtu ambaye anaweza kuiwekeza kwenye eneo ambalo linazalisha. Ile sehemu ya kumi unayojilipa iwekeze sehemu ambayo itazalisha zaidi. Iweke kwenye biashara au uwekezaji mwingine.

3.Sheria ya tatu ni UWEKEZAJI MAKINI.
Sheria hii inahitaji umakini mkubwa sana kwani fedha hung'ang'ana kwa yule ambaye anaiwekeza kwa ushauri wa watu wenye hekima.Ushauri ni kitu cha bure Mara nyingi na ndio maana Kila mtu akifahamu unayo fedha atahitaji kukushauri uzitumiaje, Wengi wamepoteza fedha kwa kukubali kupokea ushauri wa Kila mtu, kama unataka kufunguwa biashara ya kuuza nguo nenda kamfate mtu aliyeuza nguo kwa kuanzia chini na amekuwa anakua Kila siku, sehemu hii ni muhimu sana kwani ndio sehemu ambayo wengi wametapeliwa kwa kuambiwa kuna fursa wasizo zifahamu.

4.Sheria ya nne ya fedha ni HASARA KWENYE UWEKEZAJI.
Sheria hii kwa ufupi ni kwamba kama umeweka fedha zako sehemu usiyoifahamu basi fedha hiyo imepotea, kwenye kitabu cha The richest man in the Babylon tutaona kwa mifano swala hili.

5.Sheria  ya tano ya fedha ni UTAJIRI WA HARAKA
Kama una tabia ya kuwaza kwamba unaweza kutumia fedha kidogo kupata utajiri basi unajidanganya. Fedha ni matokeo ya bidii ya muda mrefu, kujituma na kushindwa kwingi lakini kamwe usitamani kupata kirahisi kwani matapeli wengi hutumia fursa hii kukuchukulia fedha zako. Kuwa na mkakati wa muda mfupi ili kukamilisha mpango wa muda mrefu.

Hizi ndio sheria tano za fedha, nenda kazifanyie kazi Nina hakika hutobaki hivyo ulivyo. Asante sana rafiki yangu.

Kinyagakelvin162@gmail.com

Kwa masomo mengine mengi yaliyopita bonyeza hapa chini;

https://kinyagakelvin.blogspot.com

0763766944/0712161251



No comments:

Post a Comment