Tuesday, 23 June 2020

Mfalme akauliza inawezekanaje watu wachache sana kuwa matajiri kuliko wengine?



Habari rafiki na ndugu yangu, bilashaka uzima ni Zawadi ambayo imetufanya Mimi na wewe tuendelee kuwasiliana na kupeana maarifa ili kustawisha fikra zetu, karibu tuwe sote....

Kama ilivyokawaida yetu siku ya jumanne tunachambuwa kitabu cha THE RICHEST MAN IN THE BABYLON na mpaka sasa tumeshajifunza mengi na kuna mengi bado hatujajifunza hivyo karibu tuweze kuona nini tunaondoka nacho na kwenda kufanyia kazi.

Jina Babeli siyo geni masikioni pako, wasomaji wa vitabu vya dini wameshasikia sana habari za babeli, babeli ulikuwa ni mji uliokuwa na utajiri mkubwa sana na hilo liliwezekana kutokana na hekima ya watu walio ishi kwenye nchi hiyo, kutoka kuwa mji wenye Kila changamoto mpaka kufikia utajiri.Hilo liliwezekana kutokana na utayari wa wananchi wa mji huo kukubali kujifunza namna ya kuupata utajiri, je na wewe upo tayari kujifunza kama watu wa babeli? Basi usiishie njiani endelea kufuatilia makala hii mpaka mwisho.

Hapo zamani alikuwepo mfalme aliyeitwa Sargon, alikuwa mfalme wa babeli na baada ya kutoka vitani anarudi na kukuta watu wake wakiteseka, kazi hakuna, wafanyabiashara hawana wateja, wakulima hawawezi kuuza mazao yao kwani watu hawana dhahabu(fedha)za kununua chakula na hali ya maisha imekuwa ngumu. Akiwa anaendelea kuongea na kansela wake wanaulizana kwamba pamoja na hali hiyo kwani dhahabu (fedha) zilizokuwepo zimekwenda wapi? Ndipo kansela wake anamjibu zimefuata mkondo wake. Jibu hili linatupa funzo kwamba kuna watu wanavutia fedha kwao,tena wakati wengine wapo kwenye matatizo makubwa wengine ndio fedha zinaelekea kwao.

Baada ya kansela kumwambia mfalme dhahabu zote zimefuata mkondo wake ndipo mfalme anauliza inawezekanaje watu wachache sana kuwa matajiri kuliko wengine? Kansela akamjibu ni kwasababu wanajua jinsi ya kupata utajiri. Ndugu pengine na wewe ulishawahi kujiuliza swali hilo la kwamba inawezekanaje wengine wawe na fedha nyingi halafu wewe huna? Sasa pengine hukujipa jibu sahihi, pengine ulijiambia ni wachawi, wana roho mbaya na kujidanganya kwamba fedha hazinunui furaha, hayo yote siyo sahihi.

Mfalme Sargon na kansela wake wanatumia hekima ya kutowaza kama wewe unavyowawazia matajiri, wakakubaliana kwamba hawa watu wachache matajiri kuna kitu wanafahamu ambacho wengi hawakifahamu hivyo ikiwezekana watafute mtu atakayewafundisha na mtu huyo hakuwa mwingine bali Arkadi, mtu aliyekuwa na utajiri mkubwa sana na uliongezeka Kila siku, basi walikubaliana aitwe na awafundishe watu wachache na hao watu wakawafundishe wengine na wengine na baadaye taifa zima litakuwa na utajiri, basi Arkad aliitwa na kuulizwa kama angeweza kufanya hivyo na alikubaliana na siku iliyofuata alianza kuwafundisha watu 100.

Kweli siku iliyofuata Arkad alikuwa mbele ya watu 100 na alianza kuwaeleza kwamba hata yeye alianzia chini kabisa mpaka alipojifunza namna ya kutunisha mifuko yake iliyo sinyaa na hapo ndipo akawaambia anakwenda kuwapa Tiba saba zitakazo kwenda kutunisha mifuko yao na atawafundisha Kila siku tiba moja mpaka siku saba watakuwa wamejifunza tiba zote.

TIBA YA KWANZA-ANZA KUTUNISHA MFUKO WAKO
Arkad alianza kwa kuwauliza Kila mmoja anajishughulisha na anayo kazi inayomuingizia kipato? Wote walikuwa na kazi zinazowaingizia kipato, Arkadi akawaambia vizuri sana kwani kama unayo kazi yoyote inayo kuingizia kipato basi unayo nafasi kubwa sana ya kuufikia utajiri.

Akamgeukia mmoja aliyesema anauza mayai na kumuuliza je kama Kila asubuhi anapokea mayai 10 na jioni unatoa tisa na moja unaacha kwenye kikapu je baada ya muda nini kitatokea?muuza mayai akajibu kikapu kitajaa mayai, Arkad akamwambia ni kweli kwasababu unachukua mayai kidogo kuliko uliyopokea.

Hivyo akawaambia tiba ya kwanza ya mfuko ulio sinyaa ni kuhakikisha Kila fedha kumi unazopokea unatumia tisa na moja uunaweka kwenye mfuko wako na baada ya muda mfuko wako utatuna na kukua zaidi. Siyo kazi rahisi ila inawezekana.

Rafiki yangu leo tuishie hapa, bilashaka dhana hii unakwenda kuianza Mara moja, Mimi rafiki yako nilijifunza tiba hii 2018 kwa mara ya kwanza na nilianza Mara moja kuifanyia kazi, mwanzo ilikuwa ngumu lakini sasa ni sehemu ya maisha yangu, kwa Kila kipato ninachopokea asilimia kumi naiweka gerezani Kama tunavyoita kisima cha maarifa kwani ukiweka ndani hazitakosa matumizi, kujua gereza la asilimia kumi tuwasiliane, Asante na siku njema tukutane wiki ijayo tuone tiba zingine zilizobaki.

Kinyagakelvin162@gmail.com

https://kinyagakelvin.blogspot.com

0763766944/0712161251
.

No comments:

Post a Comment